YESU KRISTO ANAZALIWA..JINA LAKE ATAITWA EMMANUEL MUNGU YU PAMOJA NASI
Matukio yahusianayo na kuzaliwa kwa Yesu
Kristo yameandikwa katika kumbukumbu mbili za Injili. Yanapatikana katika
Mathayo 1 na 2 na katika Luka 1 na 2. Luka atwambia kwamba matukio haya
yalitokea katika utawala wa Kaizari Augustus (Luka 2:1-2), ambayo inatuwezesha
kuthibitisha kwa usahihi kuwa Yesu alizaliwa mwaka wa nne kabla ya Kristo.
Injili ya Luka pia imeweka kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yohana Mbatizaji, na
kujitokeza kwake katika taifa, ikiweka jambo hili katika sura ya ki-historia
pia (Luka 3:1)
Tunapotafakari matukio haya tunafurahishwa
na habari kamili zinazotokana na manabii wanaotabiri makusudi ya Mungu ya
kumleta Yesu na kazi ambayo angefanya.
Unabii wa Isaya kuhusu
kuzaliwa kwa Yesu
Isaya ndiye nabii aliyepeleka ujumbe
dhahiri kwa nyumba ya Daudi akisema “Tazama bikira atashika mimba na kuzaa
mwana ambaye ataitwa Immanueli (maana yake, ‘Mungu yu nasi’)” (Isaya 7:14 ). Hili lilitimizwa mara Mariamu,
wa ukoo wa Mfalme Daudi alipomzaa mwanawe kifungua mimba Yesu kama
alivyotabiriwa katika Mathayo 1:21-23.
Pia Isaya alitabiri kazi ya baadaye ya huyu
ambaye angezaliwa akisema: “Kwa maana mtoto amezaliwa kwetu, kuna mwana ambaye
tumepewa, na ufalme utakuwa begani kwake. _ _ _ _ kuhusu utawala wake na amani
hakutakuwa na mwisho, kwenye kiti cha enzi cha Daudi na juu ya ufalme wake ili
kuufanya imara na kuutegemeza kwa njia haki na kwa njia ya uadilifu kuanzia sasa
hata milele” Isaya 9:6-7). Kutokana na utabiri huu hatuwezi kushindwa kuelewa
kuwa yesu alizaliwa ili atawale katika kiti cha Daudi wakati ufalme wake
utakaposimikwa duniani, milele.
Ujumbe wa Malaika Gabrieli
kwa Mariamu.
Malaika Gabrieli alipomtokea Mariamu,
alimwambia kuhusu kazi maalum ambayo Yesu angefanya. Maneno yake
yanamtambulisha Yesu kama
uzao wa Daudi uliotabiriwa katika 2 Samweli 7:12-16: “Na tazama utashika mimba
na kuzaa mtoto wa kiume ambaye utamwita YESU. Atakuwa mkuu na ataitwa Mwana wa
Aliye Juu Zaidi: na Bwana Mungu atampa kiti cha Enzi cha Daudi, baba yake: na
atatwala juu ya nyumba ya Yakobo, milele na kuhusu utawala wake hakutakuwa na
mwisho (Luka 1:31 -33).
Tutafakari maana ya ujumbe wa Malaika
Gabrieli kwa Mariamu.
“Utamwita YESU”, Neno Yesu katika Kigiriki
ni sawa na neno Yoshua linalopatikana katika Agano la Kale ambalo maana yake ni
“Yah (Mungu) ataokoa.” Kupitia Yesu
Mungu alikuwa analeta uokovu kutoka kwenye dhambi na mauti kwa watu wote
(Linganisha na Mathayo 1:21 )
“ataitwa Mwana wa Aliye Juu Zaidi.”
Angekuja kuwa “Mwana wa Mungu” aliyeahidiwa kwa Daudi katika 2 Samweli 7:14 (linganisha na Waebrania 1:5;
Zaburi 2:7.
“Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha
Daudi, baba yake.” Yesu ni “mzao” au mjukuu aliyeahidiwa kwa Daudi ambaye
ataanzisha upya kiti cha enzi na ufalme wa Daudi duniani (2 Samweli 7:12 -16; linganisha Isaya 9:6-7)
“Kuhusu ufalme wake hakutakuwa na mwisho”
ufalme wake hautakuwa na mwisho kwa sababu Yesu Kristo ambaye atkuwa mfalme
hafi (2 Samweli 7:16 ,
Danieli 2:44 , Ufunuo 11:15 ).
Katika mbiu fupi ya Malaika Gabrieli
tunapata maelezo dhahiri ya kazi itakayofanywa na mtoto huyu ambaye alikuwa
karibu kuzaliwa:
ü Angewaokoa binadamu katika
dhambi na mauti
ü Angekuwa Mwana wa Mungu
ü Angekuwa mwana wa Daudi, na kwa hiyo
o Angekalia kiti cha enzi cha Daudi
o Angetawala Waisraeli waliojikusanya upya
o Angeanzisha ufalme wa Mungu usio na mwisho duniani.
Jibu la Mariamu kwa mbiu ya Gabrieli
lilikuwa la unyenyekevu na ukunjufu kwa matakwa ya Mungu. Aliuliza: “Hili
litakuwaje? Maana simjui mwanaume?
Jibu la Gabrieli likawa; “Roho Mtakatifu
atakujia na uwezo wa Aliye Juu Zaidi utakufunika: kwa hiyo hicho kitu
kitakatifu kitakachozaliwa na wewe kitaitwa Mwana wa Mungu” Luka 1:34 ). Kupitia uwezo wa Roho Takatifu
ya Mungu mtoto huyu angezaliwa na kuitwa “Mwana wa Mungu” kwa utimizo wa unabii
wa Agano la kale (2 Samweli 7:14 ,
Zaburi 2:7, angalia Matendo 13:32-33, Mwanzo 3:15).
Kuzaliwa Kwake Bethlehemu
Kuzaliwa kwa Yesu Bethlehemu kulikuwa
kumetabiriwa na Nabii Micah (Micah 5:1-2) lakini Yusufu na Mariamu waliishi
Nazareti kilometa 110 kaskazini mwa Bethlehemu. Mariamu alikuwa amekaribia
kujifungua na katika hali ya kawaida ya kibinadamu ilionekana kwamba
angejifungulia Nazareti. Walakini tunaona mkono wa Mungu ukifanya kazi miongoni
mwa binadamu, kuonyesha makusudi yake (angalia danieli 4:17 ), kwa maana wakati huu Kaizari Augustus
alitoa amri kwamba dunia nzima ilipe kodi (yaani watu wote waorodheshwe). Hili
lililazimu Yusufu na Mariamu wafanye safari ndefu kwenda kwa mji wa babu zao,
Bethlehemu kwa madhumuni hayo (Luka 2:1-6) kilichoonekana kama uamuzi wa mbali
wa mtawala wa Kipagani, kilikuwa kwa kweli kimeongozwa na mkono wa Mungu katika
mashauri ya wanadamu kwa maana Yesu alikuwa azaliwe Bethlehemu (Luka 2:4-7,
Mathayo 2:4-6). Pia Micah alitabiri kazi ya baadaye ya Yesu akisema angekuwa
“Mtawala Israeli” Hili litatimizwa mpaka mpaka atakaporudi kuja kusimika ufalme
wa Mungu duniani.
Habari zenye kufurahisha
za kuzaliwa kwake.
Tukio hili lililosubiriwa kwa muda mrefu na
vizazi na vizazi vya wacha Mungu wa kuume na kike liltangazwa na malaika kwa
wachunga kondoo katika nyanda za Bethlehemu. “Msiogope; kwa maana, tazameni,
nawaletea habari njema za furaha kuu kwa watu wote. Kwenu leo hii amezaliwa
Mwokozi ambaye ni Kristo Bwana katika mji wa Daudi” (Luka 2:10 -11).
Aya
ya 10:
“Habari njema” Hii
ni tafsiri ya neno lilelile ambalo mahali pengine limeandikwa “Injili”.
“Kwa watu wote”
Habari njema inayohusiana na Yesu Kristo Bwana si kwa Wayahudi peke yao bali kwa watu wote,
Wayahudi na watu wa mataifa sawia. Hizi habari njema ni mbiu ya uwokovu ambao
Mungu ametoa kupitia kwake (Marko 16:15-16, Wagalatia 3:26-27)
Aya
ya 11:
“Katika mji wa
Daudi” Ndiyo kusema Bethlehemu, mji alipozaliwa Daudi (1 Samueli 16:1) Israeli
ilitarajia mtawala ajaye atokee katika mji huu (Micah 5:1-2).
“Mkombozi”
Mwanadamu ni mwenye mauti na dhambi na anahitaji kukombolewa kutoka katika
kifo. Kupitia kwa Yesu Kristo Mungu ametupatia msamaha wa dhambi na matumaini
ya kuchangia kutokufa na kristo wakati atakaporudi duniani (2 Timoteo 1:10; 1
Wakorinto 15:21-23, 51-54) kwa hiyo Yesu ni “Ukombozi wa mwanadamu utokao kwa
Mungu.”
Wanajimu Kutoka Mashariki.
Miongoni mwa wale waliokuwa wamesoma unabii
na kutarajia kuzaliwa kwa Kristo wakati huo ni “Wanajimu kutoka sehemu za Mashariki.”
Mara tu walipofika Yerusalemu walianza kuuliza. “Yuko wapi yule aliyezaliwa
akiwa mfalme wa Wayahudi?” (Math. 2:2) walielewa kutokana na Manabii kuwa
hatima ya mtoto aliyezaliwa ni kuwa Mfalme wa Wayahudi akikalia kiti cha enzi
cha Daudi (2 Samweli 7:12 -14;
Isaya 9:6-7)
Herode aliposikia udadisi wa Wanajimu
alifadhaika na kuita Makuhani na Waandishi na “kuwataka wamwambie ni wapi
Kristo alipokuwa amezaliwa” (Math. 2:4), walijua jibu mara moja kutokana na
Nabii Micah wakamjibu: katika Bethlehemu ya Yuda (Micah 5:2; Math. 2:5-6).
Kutokana na hili twaona kuwa Wayahudi
walifahamu kwamba:
ü Kristo angezaliwa
ü Katika Bethlehemu
ü Na angetawala “watu wangu Israeli.”
Yesu Mwana wa Mungu na
Mwana wa Binadamu.
Majina haya mawili, “mwana wa Mungu” na
“Mwana wa Binadamu” yanatumika katika kumbukumbu zote za Injili. Yanaonyesha
kuwa Mungu alikuwa baba yake na wakati huo huo akiwa mzao wa Adam alihusiana na
mwanadamu ambaye yeye alikuja kuokoa. Tunaona hizi nasaha mbili zikitangazwa na
Gabrieli katika maneno yake kwa Mariamu. Angekuja kuwa “Mwana wa Aliye Juu
Zaidi” yaani wa Mungu na angekalia “kiti cha enzi cha Daudi, baba yake” (Luka
1:32; 2 Samweli 7:12-14; Matendo 2:30).
Paulo asema “Wakati ulipotimia “Mungu
alimtuma mwanaye aliyezaliwa na mwanamke katika sheria” (Wagalatia 4:4) kuhusu
mwanae Mungu aliweza kusema “Wewe ni mwanangu, leo hii nimekuzaa” (Zaburi 2:7,
Waebrania 1:5; 5:5)
Ingawa kuzaliwa kwa Yesu kulibashiriwa muda
mrefu na manabii kuwepo kwake kulianza mara Mungu kupitia Roho Yake Takatifu
aliposababisha Mariamu kubeba mimba, miaka 2000 iliyopita (Luka 1:35 )
Nabii Isaya anataja kuzaliwa kwa Yesu
Kristo Bwana kwa jinsi hii: “Na yeye
(mungu) aliona kuwa hapakuwa na yeyote, na kuwaza kwamba hapakuwa na mtetezi:
kwa hiyo mkono wake ukaleta uwokovu kwake” (Isaya 59:16).
Mungu kwa kuona hali ya dhambi za binadamu
na kwa kujua kwamba hapakuwa na yeyote ambaye angeonyesha utii mkamilifu au
kumwokoa mwanadamu katika utumwa wa dhambi na mauti, alichukua hatua ya kumpata
mtu ambaye kwa kupitia kwake angeleta uokovu.
Alimtia nguvu huyo aliyezaliwa na mwanadamu ili ashinde dhambi na
mauti na hiyo kufungua njia ya wokovu na
uhai kwake mwenyewe na wengine wote ambao wangekuja kwa mungu kupitia kwake, “
kazi ya mwana wa Adamu imeainishwa
katika Waebrania 2:6-18.
Ulazima wa mungu kujihusisha na wokovu wa mwanadamu kutoka
katika dhambi ulitabiriwa tangu mwanzo, Aliposema “uzao wa mwanamke”
ungekiponda kichwa cha “nyoka” kuonyesha
kwamba Mungu angemfunika mwanamke kwa kivuli chake ili azae mwana ambaye
angevunja nguvu ya dhambi ya nyoka Mwanzo 3:15;
Waebrania 2:14, Wagalatia 4:4)
No comments:
Post a Comment