Tuesday, 16 December 2014

JE UNAFAHAMU MAANA YA KUMSIFU NA KUMWABUDU MUNGU?

SOMO LA SIFA NA KUABUDU
                                                  SEHEMU YA TANO 
              MAANA YA KUMSIFU NA KUMWABUDU MUNGU.
Nini maana ya kusifu na kuabudu?
Kumsifu na kumwabudu Mungu, ni kitendo cha mtu kumtukuza, kumhimidi, kumwinua, kumwadhimisha, kumshukuru na kumheshimu Mungu kwa vile alivyo na kwa yale aliyoyatenda. (Appreciation and admiration for who He is and for what He has done.)

Tafsiri za maneno; Kushukuru, Kusifu na Kuabudu.

a)      Kumshukuru Mungu;- Ni kumueleza Mungu jinsi tunavyothamini wema wake, fadhili  
                                               zake na baraka zake kwetu.

b)     Kumsifu Mungu;                 - Ni kumueleza Mungu matendo makuu na ya ajabu aliyoyafanya.
                                               Au ni kuwaeleza wengine matendo makuu ya Mungu.

c)      Kumwabudu Mungu; - Ni kumueleza Mungu tukuzo zetu, heshima yetu na upendo  
                                        wetu wake kwa uzuri wa tabia zake kwetu.
                                        (Credentials and Characters).
                             
Namna za kumsifu, na kumshukuru na kumwabudu Mungu.
Katika maisha yetu sisi kama waumini, tumezoea kumshukuru, kumsifu na kumwabudu Mungu kwa njia kuu zifuatazo;
1.   Kumwimbia nyimbo za shukurani, sifa na kuabudu
2.   Kumweleza kwa maneno, shukurani, sifa na maneno ya kumwabudu
3.   Kumtolea Mungu sadaka na dhabihu mbalimbali kwa upendo wake mkuu

Haya mambo matatu, kusifu, kushukuru na kuabudu, ni mambo yanayofanana sana. Inaweza ikawa vigumu kuyatenganisha na kukikanya kitu kimoja wapo pasipo wenzake, kwasababu ni mambo yanayokwenda kwa pamoja. Lakini hapa chini, nataka nijaribu kuvitenganisha kwa maelezo tu, japo inaweza ikawa vigumu sana kukifanya kimoja bila wenzake.

Nini maana ya Kushukuru.
Kushukuru ni kitendo anachofanya mtu, cha kuonyesha kupenda, kufurahia na kuthaminikitendo fulani alichofanyiwa na mtu mwingine. Nasi tunatakiwa kumshukuru Mungu, kwasababu, Mungu ametufanyia mambo mengi sana, yanayoonyesha upendo wake na wema wake kwetu. Kwasababu ya fadhili nyingi anazotufanyia Mungu, tunatakiwa kumwonyesha jinsi tunavyofurahia, jinsi tunavyopenda na jinsi tunavyothamini wema wake huo katika maisha yetu. Kwahyo, kushukuru ni kitendo anachofanya mtu, cha kuonyesha kupenda, kufurahia na kuthaminikitendo fulani alichofanyiwa na mtu mwingine. 

Nini maana ya Kusifu.
Kusifu ni ile namna ya mtu kuelezea matendo makuu ya Mungu. Unapotaka kumsifu Mungu, ni muhimu utafakari na ujue mambo ambayo Mungu amayafanya, kwasababu Kumsifu Mungu ni ile namna ya mtu kuelezea matendo makuu ya Mungu, aliyoyafanya. Kwa mfano; Mtu anaposema Mungu, wewe ndiwe uliyeumba vitu vyote, ndiwe unayetupa nguvu na afya, ndiwe unayetulisha na kutunywesha … n.k. Hapo mtu wa Mungu huwa katika hali ya kumsifu Mungu, kwasababu kusifu ni kueleza matendo ya Mungu. Unaposema Mungu, wewe ndiwe iliyefungua bahari ya Shamu, ndiwe uliyevinja kuta za Jeriko, ndiwe Mungu uliyewalisha Waisraeli kwa mvua ya mikate, hakika hakuna Mungu kama wewe…  hapo utakuwa unamsifu Mungu, na sio kumwabudu Mungu, kwasabubu kusifu ni kutaja matendo ya Mungu.

Kusifu na Kushukuru ni mapacha
Kusifu na kushukuru ni vitu vinavyokwenda kwa pamoja, haviachani; ni namna zinazokwenda pamoja. Ninasema hivi kwasababu, haiwezekani mtu akaweza kushukuru, pasipo kueleza anashukuru kwa ajili ya nini au kwa ajili ya tendo gani. Kwahiyo, mtu anapoanza kushukuru, shukurani ile huwa inafuatiwa na tendo fulani lililofanyika kwa mtu huyu, lililomfanya aamue kutoa shukurani zake. Na mtu anapoanza tu kueleza matendo mazuri au makuu yaliyofanyika, hapo mtu huwa ameingia katika sifa au katika kusifu. Kumbuka kwamba, kusifu ni namna ya mtu kueleza matendo ya mtu au mambo aliyoyafanya. Kwahiyo, mtu anapoanza kushukuru, shukurani ile huwa ina sababu. Ile sababu ikiajwa, basi basi kusifu hutakuwa kumeingia katika kushukuru. Ndio maana nimesema kwamba, kusifu na kushukuru ni mapacha, haviachani, bali vinakwenda kwa pamoja.

Kwa mfano; mtu anasema ‘Mungu nakushukuru kwa ulinzi wako’ uaweza kuona kwamba, shukurani ya mtu huyu, imesukumwa kutoka moyoni mwake, kwasababu ya tendo la ulinzi ambalo Mungu amelifanya kwake. Au mtu anasema ‘Mungu nakushukuru kwa uponyaji wako’ unaweza kuona wazi wazi kwamba, tendo la uponyaji ambalo Mungu amelifanya kwa mtu huyu, ndilo lililosukuma moyo wa huyu mtu kumpa Mungu shukurani. Kwahiyo, shukurani na sifa, ni vitu vinavyokwenda pamoja, ni mapacha. Kwahiyo, ninaweza kusema kwamba, kila kushukuru ni kusifu, lakini si kila kusifu ni kushukuru. Hii ina maana kwamba, kila kushukuru huwa kunabeba sifa pia kwa ndani, lakini si kila kusifu huwa kunabeba kushukuru ndani yake.

Nini maana ya Kuabudu
Kama tulivyoona hapo nyuma, Kuabudu ni ile namna ya kueleza jinsi Mungu alivyo; ni ile namna ya mtu kueleza tabia za Mungu. Pale mtu anaposema wewe Mungu ni Mtakatifu, ni wa milele, hauna mwanzo wala mwisho, akili zako hazichunguziki, n.k. Hapo mtu wa Mungu anakua anamwabudu Mungu, kwasababu ammekuwa akimweleza Mungu juu ya tabia zake na sio matendo yake. Mungu kuwa Mtakatifu, si tendo, bali na hali au tabia ambayo anayo siku zote. Kwahiyo, mtu anapoeleza matendo makuu ya Mungu, huwa anakuwa anamsifu Mungu; lakini pale mtu anapoeleza tabia za Mungu, hapo anakuwa anamwabudu Mungu.

Unaweza kwenda mbele za Mungu kumwambia jinsi aliyo mpole, na si mwepesi wa hasira. Unaweza pia kumwambia jinsi alivyo mwaninifu, jinsi alivyo mzuri, jinsi alivyo mkuu, n.k. Haya yote, si matendo ya Mungu, bali ni tabia za Mungu; ni vile Mungu alivyo kwetu. Kama nilivyosema hapo juu kwamba, haya mambo, yanayofanana sana; na tena inaweza ikawa vigumu kuyatenganisha wakati unapokuwa mbele za Mungu.  Si rahisi kukiyafanya kimoja, pasipo wenzake, kwasababu ni mambo yanayokwenda kwa pamoja.

Lakini hapa juu, nimejaribu kuvitenganisha kwa maelezo tu, japo inaweza ikawa vigumu sana kukifanya kimoja bila wenzake. Nia yangu si kukufanya utumie kimoja bila wenzake, hapana! Nimejaribu kuvitenganisha hivi, ili kukupa uelewa wa kina tu, lakini haya mambo matatu, shukurani, sifa na kuabudu, huwa ni vitu vinavyokwenda kwa pamoja, wakati mtu anapokuwa katika maombi au anapokuwa katika uwepo wa Mungu, hata kama hakwenda kwa nia ya kuomba kitu.  {Zaburi 33.}
Huu ni mwendelezo wa somo la Sifa na Kuabudu....



No comments:

Post a Comment