Friday, 21 November 2014

SOMO: KWANINI KUSIFU NA KUABUDU


KWANINI KUSIFU NA KUABUDU
utangulizi
Zaburi  100:1-5  
            “1Mfanyieni Bwana shangwe dunia yote; 2Mtumikieni Bwana kwa furaha, njooni mbele zake kwa kuimba; 3Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu, ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake, tu watu wake na Kondoo wa malisho yake. 4Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru, nyuani mwake kwa kusifu, mshukuruni lihimidini jina lake5Kwa kuwa Bwana ndiye mwema, rehema zake ni za milele, na uaminifu wake, vizazi na vizazi.

Zaburi 146: 1-2
1Haleluyah. Ee nafsi yangu, umsifu Bwana. 2Nitamsifu Bwana,
muda ninaoishi,  nitamwimbia Mungu wangu ningali ni hai.”

Mtumishi wa Mungu, Mfalme Daudi, anaandika Zaburi hizi kwa ufunuo alioupata, juu ya kusudi la Mungu kwa wanadamu. Mfalme Daudi alipewa kuelewa kwamba, sisi wanadamu wote ni kazi ya mikono ya Mungu, na tumeumbwa ili kumtolea Mungu sifa na ibada, siku zote za maisha yetu. Mfalme Daudi alipopata ufunuo huu na kuelewa jambo hili, akaandika Zaburi hizi tulizozisoma, ili kutufahamisha na kutuhamasisha watu wote, kumsifu na kumwabudu Mungu, kwani ndio wito wetu mkuu. Lakini ukiangalia jinsi wanadamu wengi tunavyoishi, utagundua kwamba, si watu wengi waliopo duniani, wameelewa kitu ambacho Mfalme Daudi alielewa; si watu wengi tunaoishi, tumeelewa kusudi hili la Mungu juu ya Maisha yetu, kwamba sisi wote ni viumbe wa kumsifu na kumwabudu Mungu wetu.

Si watu wengi wanaoelewa kwamba, sisi binadamu ni vyombo maalumu vya kumpa Mungu sifa na ibada. Na ndio maana watu wengi huwa hawana desturi ya kumwabudu Mungu kila siku. Watu wengi angalau wanamwabudu Mungu kwa kiasi katika maisha yao, ni wale wanaomwabudu Mungu mara moja kwa wiki; ni watu ambao huwa wanaosubiri mpaka ifike siku maalum iliyopangwa kwa ajili ya ibada, kwa mfano siku ya Jumapili, ndipo utawaona wana kazana kwenda makanisani kusali.


Lakini laiti kama wangejua kwamba, Mungu anatarajia na anatazamia sana, watu wake tuwe tunakutana naye kila siku katika ibada za binafsi, basi watu wengi zaidi wangekuwa na desturi ya kumwabudu Mungu kila siku katika nyumba zao au vyumbani mwao. Tatizo kubwa la watu wengi ni kutokujua; na ndio maana watu wengi hawapatikani ibadani; hata katika nyumba zao, watu wengi hawana muda wa kukaa mbele za Mungu, ili kumsifu na kumtukuza muumba wao, kila siku baada ya kazi zao kwisha. Bali watu wengi huwa wanaosubiri mpaka ifike siku maalum ya kwenda ibadani, kwa mfano siku ya Jumapili, ndipo utawaona wanajiandaa na kwenda kusali. Hii si sawa. Jamani, kwa wale ambao mlikuwa hamfahamu, basi ni muhimu sana ujue kwamba, sisi binadamu na viumbe wote, ni vyombo maalumu vya kumpa Mungu sifa na ibada kila siku.  Hii ndio sababu ya sisi kuumbwa na kuishi.


Lakini, cha ajabu ni kwamba, watu wengi huwa hawafanyi bidii sana kutenga muda au kutafuta muda wa kukaa mbele za Mungu na kumsifu na kumwabudu yeye. Hali hii inatokana na kutoelewa kwamba, binadamu tumeumbwa kama vyombo maalum vya kumsifu na kumwabudu Mungu, kila siku. Na ndio maana Mfalme Daudi alipewa ufunuo huu na Mungu, ili tuweze kujua kwamba, sisi binadamu wote na viumbe vingine vyoote, ni vyombo maalumu vya kumpa Mungu sifa na ibada kila siku.  Hii ndio sababu ya sisi kuumbwa na kuishi.


Na Mfalme Daudi alijaliwa kulielewa jambo hili, na ndio maana kila wakati alitembea na kinubi chake, akimsifu Mungu wake nyakati zote. Biblia inatuambia kwamba, Daudi alikuwa mchunga mbuzi, kondoo na ng’ombe wa babake; lakini na huko porini nako, Daudi alikuwa akichunga wanyama wake huku akimwimbia Mungu wake kwa furaha, akimpigia na muziki kwa kinubi chake. Daudi alielewa kusudi la Mungu juu ya maisha yake. Pamoja na majukumu mengi aliyokuwa nayo, lakini bado Mfalme Daudi alijitahidi kuishi maisha ya ibada, bila kujali mazingira aliyokuwepo.

Ni muhimu tujue kwamba, Mungu ametuumba sisi na viumbe wote, ili tutimize mapenzi yake au matakwa yake au mahitaji yake, amabyo ni kusifiwa na kuabudiwa. Hii ina maana kwamba, Mungu anataka kusifiwa na Mungu anataka kuabudiwa. Kwa Mungu, sifa na ibada ni vitu vya muhimu sana, Mungu anaheshimu sana sifa na ibada. Na Mfalme Daudi alilielewa kusudi hili la Mungu juu ya maisha yake, kwamba yeye ameumbwa awe kama chombo cha kumsifu na kumwabudu Mungu siku zake zote za maisha yake, maadam anaishi. Na Biblia inasema kwamba Daudi alilitimiza kusudi hili vizuri. Na ndio maana tunaona anaandika katika kitabu cha Zaburi zake kwamba;
1Halleluyah! Ee nafsi yangu, umsifu Bwana. 2 (Nami Daudi) Nitamsifu Bwana, muda ninaoishi, nitamwimbia Mungu wangu ningali ni hai.”
                                             Zaburi 146: 1-2

Si watu wengi wanaojua kwanini Mungu anaheshimu sana na anapenda sana ibada na sifa. Na hivyo basi, si watu wengi wanaojua kwanini Mungu anataka na ameagiza kusifiwa. Na ndio maana Mungu amanipa ufunuo huu, ili nikuandikie, ili nawewe uweze kulijua kusudi la Mungu maishani mwako na maishani mwetu sote. Nataka na wewe upate ufunuo huu, ili upate kujua sababu inayomfanya Mungu kuheshimu sana sifa na ibada. Katika kitabu hiki, utaelewa jinsi ambavyo Mungu anaishi katika sifa za watu wake, yaani jinsi Mungu anavyoishi katika sifa na ibada, kama vile Mfalme Daudi anavyoandika katika kitabu cha Zaburi 22:3 kwamba; “Wewe U Mtakatifu, Uketiye juu ya sifa za Israeli.”

Kwahiyo, katika sura hii ya kwanza, tumeona kwamba, tatizo kubwa la watu wa Mungu linatokana na kutokujua. Tumeona kwamba, si watu wengi wanaoelewa kwamba, sisi binadamu ni vyombo maalumu vya kumpa Mungu sifa na ibada. Na ndio maana watu wengi huwa hawana desturi ya kumwabudu Mungu kila siku. Na tumeona kwamba, watu wachache ambao angalau wanamwabudu Mungu kwa kiasi katika maisha yao, ni wale wanaomwabudu Mungu mara moja kwa wiki; ni watu ambao huwa wanaosubiri mpaka ifike siku maalum ya ibada, kwa mfano siku ya Jumapili, ndipo utawaona wana kazana kwenda makanisani kusali.

Hii inatokana na kutokujua; na kama watu wanajua hili, basi hawafanyi wanachotakiwa kufanya kwasababu ya uzembe tu na kutokutii. Lakini laiti kama wangejua kwamba, Mungu anatarajia na anatazamia sana, watu wake tuwe tunakutana naye kila siku katika ibada za binafsi, basi watu wengi zaidi wangekuwa na desturi ya kumwabudu Mungu kila siku, huko katika nyumba zao au kule katika vyumba vyao. Kwahiyo tunaweza kusema kwamba, kutokukutana na Mungu mara kwa mara katika ibada, kunatokana na kutokujua (ujinga) na pia, uzembe na kutokutii; ndio maana watu wengi hawapatikani ibadani. Wewe waangalie watu wengi wanavyoishi katika nyumba zao, nakwambia, watu wengi hawana muda wa kukaa mbele za Mungu, ili kumsifu na kumtukuza Mungu wetu. Kila siku baada ya kazi zao kwisha, watu hutumia muda mwingi sana katika kuangalia TV na katika kutembeleana na kupiga soga.
Utakuta watu wanaweza kukaa katika soga na katika TV, kwa masaa mengi. Swala la kumtumikia Mungu kwa sifa na ibada, halipo katika ratiba zao za kila siku. Ibada imekuwa kitu cha mara moja kwa wiki; watu wengi huwa wanaosubiri mpaka ifike siku maalum ya kwenda ibadani, kwa mfano siku ya Jumapili, ndipo utawaona wanajiandaa na kwenda kusali. Jamani, hii si sawa. Kwahiyo, kwa wale ambao mlikuwa hamfahamu, basi nimewaandikia kitabu hiki, tena kwa umuhimu sana, ili ujijue kwamba, wewe ni chombo cha ibada mbele za Mungu. Ni muhimu sana tujue kwamba, sisi binadamu na viumbe wote, ni vyombo maalumu vya kumpa Mungu sifa na ibada kila siku.  Hii ndio sababu ya sisi kuumbwa na kuishi.

Na ndio maana Mfalme Daudi alipewa ufunuo huu na Mungu, ili tuweze kujua kwamba, sisi binadamu wote na viumbe vingine vyoote, ni vyombo maalumu vya kumpa Mungu sifa na ibada kila siku. Jamani, hii ndio sababu kubwa na ya kwanza, kwanini sisi tupo duniani. Na Mfalme Daudi alijaliwa kulielewa jambo hili, na ndio maana kila wakati alitembea na kinubi chake, akimsifu Mungu wake nyakati zote. Pamoja na majukumu mengi aliyokuwa nayo, lakini bado Mfalme Daudi alijitahidi kupata muda wa kumsifu na kumwimbia Mungu.

Jamani, Daudi anatufundisha jambo kubwa sana hapa. Yaani pamoja na majukumu mengi aliyokuwa nayo kama Rais wa nchi, lakini bado Mfalme Daudi alijitahidi kupata muda wa kuishi maisha ya ibada, bila kujali mazingira aliyokuwepo. Najaribu kupiga picha mawazoni kwangu, jinsi Daudi alivyokuwa akizama katika sifa na ibada. Napiga picha jinsi alivyokuwa akitembea huku akiimba. Naweza kuona jinsi Daudi alivyokuwa akiswaga wanyama wake huku akiimba nyimbo za kumsifu Mungu wetu. Naona jinsi ambavyo alikuwa akifua nguo huku midomo yake ikibubujisha sifa. daudi alikuwa akipika chakula huku akimsifu Mungu. Daudi alikuwa akifagia nyumba au banda la kuku au zizi la ngómbe huku akimsifu Mungu.

Na kwa wale mlioko maofisini, hamna jambo la kujitetea, mwenzenu Mfalme Daudi pia, alikuwa akifanya kazi za kuandika huku akimnong’oneza Mungu maneno ya sifa. Jamani, huyu alikuwa Rais wa nchi, tena ni nchi yenye vita nyingi na mapigano makaki, kushoto na kulia, mpaka hivi leo! Sembuse wewe ambaye hata Ukatibu kata hauna! Lakini pamoja na kwama alikuwa kiongozi wa nchi nzima, bado pamoja na ubize (busy) wote aliokuwa nao, na mapigano yote waliyokuwa nayo, bado Mfalme Daudi alijitahidi kupata muda wa kujihudhurisha na kukaa katika uwepo wa Mungu na kumsifu na kumwimbia Mungu wetu. Na kwa saluti kabisa mimi ninampongeza sana kwa kusema, Mheshimiwa Mfalme Daudi alikuwa chombo cha sifa! Jamani, ni muhimu tujue kwamba, Mungu anaishi katika sifa za watu wake. Mungu anaishi katika sifa na ibada, kama vile Mfalme Daudi alivyoandika katika Zaburi 22:3 kwamba; “Wewe U Mtakatifu, Uketiye juu ya sifa za Israeli.” Hivyo, Mungu ametuumba sisi na viumbe wote, ili tutimize mapenzi yake au matakwa yake au mahitaji yake, amabyo ni kusifiwa na kuabudiwa. (Hii nitakuelewesha vizuri katika sura inayokuja). Ndio maana Mungu anataka sana kusifiwa na kuabudiwa. Kwa Mungu, sifa na ibada ni vitu vya muhimu sana.

Kwakweli, Mungu anaheshimu sana sifa na ibada. Na Mfalme Daudi alilielewa kusudi hili la Mungu juu ya maisha yake, kwamba yeye ameumbwa awe kama chombo cha kumsifu na kumwabudu Mungu siku zake zote za maisha yake, maadam anaishi. Na Biblia inasema kwamba Daudi alilitimiza kusudi hili vizuri. Mfalme Daudi alijitahidi kupata muda wa kujihudhurisha na kukaa katika uwepo wa Mungu na kumsifu na kumwimbia Mungu wetu. Na kwa saluti nyingine, ninapiga huku nikisema, Mheshimiwa, His Excellency, President, Daudi wa Yese, alikuwa chombo cha sifa mbele za Mungu!      SOMO LITAENDELEA


















No comments:

Post a Comment