Friday, 30 January 2015

JICHO LA MBALI WIKI HII :MAHOJIANO NA JENNIFER MGENDI

JICHO LA MBALI WIKI HII NA JENNIFER MGENDI

 

Akiwa tayari na albamu zisizopungua tano kibindoni, Jennifer Mgendi(pichani) ni miongoni mwa wanamuziki wa muziki wa injili au kwa kiingereza Gospel nchini Tanzania ambao wamejijengea sifa na umaarufu mkubwa kutokana na kazi yake hiyo ya uimbaji na kumtukuza mola. 
Lakini tofauti moja kubwa ya Jennifer na wanamuziki wengine wa muziki wa injili ni kwamba yeye pia ni mtunzi mzuri wa hadithi za filamu.Baadhi ya filamu alizowahi kutunga ni kama vile Pigo la FarajaJoto la Roho na Teke la Mama. 

Alianza rasmi kujishughulisha na kazi ya muziki wa injili mwaka 1995.Albam yake ya kwanza iliitwa ‘Nini?’. Baada ya hapo alitoka tena na albamu zake zilizokwenda kwa majina ‘Ukarimu wake’, ‘Yesu Nakupenda’,'Nikiona Fahari’ na ya hivi karibuni zaidi inayoitwa Mchimba Mashimo. 

Hivi karibuni tulipata nafasi ya kufanya naye mahojiano ambayo utayasoma hivi punde. Katika mahojiano haya,Jennifer anakupa kwa undani kuhusu historia yake kimuziki na kibinafsi. Ni kweli kwamba muziki wa injili wa leo ni wa “kidunia” zaidi ya “kiroho”? Anasemaje kuhusiana na hoja hiyo? Je Jennifer anaongeleaje tofauti za muziki wa injili na ule wa Bongo Fleva?Unakubaliana naye? 

Nini mipango yake kwa mwaka huu wa 2009 na ana ushauri gani kwa vijana?Fuatana nasi katika mahojiano yafuatayo; 


FTBLOG: Karibu Jennifer ndani ya FPCTTEGETA  BLOG. bwana asifiwe?
JM:Amen…
FTBLOG:Kwa kifupi tu unaweza kutueleza historia ya maisha yako?
JM:Nilizaliwa miaka karibu 37 iliyopita hapa hapa jijini Dar es Salaam katika familia ya watoto watatu nikiwa nimetanguliwa na kaka wawili. Nimepata elimu yangu katika mikoa ya Dar es salaam na Tanga. Nilianza uimbaji rasmi mwaka 1995 na hapo katikati nilifanya kazi kadhaa za kuajiriwa kama Ualimu na Ukutubi lakini tangu mwaka 2007 niliacha kazi za kuajiriwa na mpaka hivi leo ninafanya shughuli zangu binafsi.
FTBLOG:Mara nyingi wasanii huwa wanaanza kwa kufuata mfano wa mtu,watu au kitu fulani.Kwa upande wako nini kilikushawishi uingie kwenye muziki wa injili.Je kwenye muziki wa injili ndiko ulikoanzia au ulianzia kwingine halafu ndio ukahamia kwenye injili?
JM:Watu wengi walikuwa wakinivutia sana na kunihamasisha kwa habari ya uimbaji lakini miaka hiyo nilivutiwa zaidi na Jim Reeves na Yvonne Chakachaka ambao walikuwa wananivutia sana.
Nimeanza moja kwa moja kuimba muziki huu wa injili kwa sababu tayari injili (ambayo ni uweza wa Mungu uletao wokovu kwa kila aaminiye) ilikuwa imebadilisha maisha yangu. Kwa hiyo sina mwingine wa kumwimbia zaidi ya huyo mwenye Injili yaani Yesu Kristo.
FTBLOG:Kwa faida ya wale ambao hawajafuatilia kwa ukaribu kazi zako,mpaka hivi sasa umeshatoa albamu ngapi,zinapatikana wapi na wewe kama msanii wa muziki wa injili unafanyia wapi kazi zako?
JM:Mpaka sasa nina albam tano za kusikiliza ambazo ni Nini?,Ukarimu WakeNikiona FahariYesu Nakupenda na Mchimba Mashimo. Pia nina video za nyimbo ambazo ni Yesu Nakupenda na Mchimba Mashimo. Hali kadhalika nina matoleo ya filamu ambayo ni Joto la Roho, Pigo la Faraja na Teke la Mama. Sina sehemu maalum ninayofanyia shughuli zangu kwani shughuli zangu sio za kukaa sehemu moja.
FTBLOG:Kumekuwepo na ukosoaji kwamba ninyi waimbaji wa muziki wa injili wa kizazi hiki mnapoteza kabisa uhalisia wa muziki huo.Wanaosema hivyo wanasema kwamba muziki wenu hauna vionjo vya “kiroho” bali umejaa vionjo vya “kidunia” kutokea kwenye midundo yake na wakati mwingine hata kwenye mashairi au ujumbe uliomo.Unasemaje kuhusu ukosoaji huo?
JM:Unajua ndugu yangu siwezi kukanusha wala kukubaliana na hoja yao hiyo. Inawezekana ni kweli wanavyosema na hii inatokea zaidi pale waimbaji tunapokosa kiasi. Hata hivyo “kiroho” kwa mtu mmoja kwa mwingine chaweza kuwa ni “kidunia”.
Kuna watu wengine hata kupiga makofi tu wakati unaimba kwao ni “kidunia”. La muhimu ni kwamba mradi mashairi na ujumbe unampa Mungu sifa na utukufu, binafsi sioni ubaya wowote wa nyimbo za injili kuwa na “midundo” na wala sijawahi kusoma kwenye biblia sehemu inayokataza kupiga midundo sanasana nimesoma Zaburi ikisema “….pigeni kwa ustadi…”.
Kuhusu ujumbe wa kidunia kwa kweli mimi sijasikia mwimbaji wa nyimbo za injili akiimba nyimbo za kidunia maneno yote tunayoimba yamo kwenye biblia au angalau hayapingani na mafundisho ya msingi ya biblia.
FTBLOG: Mara kwa mara kumekuwepo watu ambao aidha wanajaribu kukufananisha na waimbaji wengine wa muziki wa injili kama Rose Mhando,Bahati Bukuku na wengineo.Wengine wamethubutu hata kuwapambanisha.Je uhusiano wako na wanamuziki wengine wa injili ukoje?Mnajiona kama washindani au washirika katika Bwana?
JM:Ni kweli mara zingine wanafanya hivyo lakini nadhani kimsingi tunatofautiana na kila mmoja ana uimbaji wake kwa kadiri ya kipawa au kipaji alichopewa na Bwana. Ila la kufurahisha ni kwamba hatuna tabia ya kushindana kwani kila mmoja kapewa karama kivyake na kubwa zaidi ni kwamba tunatambua kuwa wote lengo letu ni moja, yaani kuujenga ufalme wa Mungu hapa duniani. Kwa hiyo huwa tunashirikiana sio jukwaani tu bali mara nyingine hata katika mambo ya kawaida ya maisha.
FTBLOG: Kwa muda sasa umekuwa mwanamuziki.Unadhani ni mambo gani matatu ya msingi ambayo umejifunza kutokana na kazi yako ya muziki na ambayo unadhani usingeyajua kama usingekuwa mwanamuziki?
JM:1. Nimejifunza nchi yangu na kuifahamu zaidi kwani nimesafiri sana katika mikoa na wilaya nyingi ambazo nisingefika kama sio muziki.
2. Nimejifunza mambo mengi sana yaliyonijenga kiroho kutokana na kualikwa kuhudhuria mikutano, semina na makongamano ya kiroho.
3.Nimejifunza kuishi aina fulani ya maisha yenye kiasi fulani cha nidhamu kutokana na nafasi yangu katika jamii, maisha ambayo pengine nisingekuwa maarufu nisingeishi hivyo.

No comments:

Post a Comment