SARAH K ni muimbaji anayegusa watu wengi hasa kutokana na nyimbo
anazoziimba, lakini ni wachache sana wanaofahamu historia ya muimbaji huyo.
Muimbaji huyo aliyezaliwa miaka 42 iliyopita, ameolewa na
mchungaji japo kabla ya kuanza huduma ya uimbaji, alishafanya jitihada nyingi
maishani ikiwemo kuuza mbogamboga ili mradi maisha yasonge.
Makala haya yanaangazia maisha na mapito magumu aliyoyapitia
muimbaji huyo kabla ya kuinuliwa na Mungu.
Mwimbaji wa nyimbo za injili Sarah K
Kabla ya kuanza huduma ya uimbaji, Sara ambaye jina lake kamili
ni Sarah Kiriare alikuwa akikusanya fedha kidogokidogo ili apate kuingia
studio, ambapo alikuja kufanikiwa na kutoa albamu kwa lugha yake ya asili.
Mbali ya changamoto mbalimbali alizowahi kupitia ikiwemo
kukatishwa tamaa na baadhi ya rafiki zake tena wa karibu, ikiwemo kudai kwamba
sauti yake haifanani na uimbaji na kwamba ni kama vile anaongea na si kuimba na
pia wengine wakisema sauti yake ni ya kiume, jambo ambalo kwa kweli
lilimhuzunisha sana, lakini yote hayo hayakumzuia kusonga mbele.
Pamoja na kudharauliwa na kuonekana hafai kwa baadhi ya waimbaji
ambao kwa namna moja au nyingine amewafanya kujulikana mbele ya jamii, pia ni
jambo ambalo Sarah anaguswa nalo moja kwa moja.
Sarah anasema kuwa suala la kudharauliwa lilikuwa likimliza na
kuamua kumlilia Mungu hadi kufikia hapo alipo; ni matokeo ya kusema jambo
linamlomsumbua kwa Mungu wake, mathalan msanii mmoja aliyewezeshwa kupitia
Sarah, na kisha baada ya hapo maneno yakaanza, ikiwamo kudai kuwa Sarah si
lolote wala si chochote kwa maana hajawika kama ambavyo muimbaji huyo
aliyewezeshwa kutoka anavyowika.
Mwimbaji wa nyimbo za injili nchini Kenya Sarah K.
Muimbaji huyo ameshawahi kuuza nyanya, magunia, kutembea kwa
mguu kwa kukosa nauli, kuimba kwa kukopa pesa ya studio na albamu haitoki
kutokana na kuwa na deni kubwa, kutembeza kanda mguu kwa mguu.
“Niseme tu nimeshapitia maisha magumu; nimeshauza nyanya,
nimeuza sukuma, nimeuza mangurunya, nimetembea mguu yaani kwa miguu bila ya
kupata hela ya kwenda na gari.
“Nimeanza kuimba kwa kukopa pesa; naomba pesa za studio; naenda
halafu siuzi kwa hivyo nadaiwa hizo fedha sijui nizitoe wapi.
Nimeshalia, nimeshatembeza kanda zangu zikiwa mfukoni nikipeleka
kwa wenye maduka yaani mambo yalikuwa magumu mpaka mahali Mungu akanifikisha
nasema asante.”
Sarah K ameolewa na ana watoto watatu na anasema kuwa yeye ni
Mkenya; anaeleza sababu za watu wengi kulia akiimba nyimbo zake: “Nimeshaona
hivyo tena mara nyingi nikienda kwenye kanisa ambako ninakwenda kuhudumu,
ninajikuta hata mimi mwenyewe nalia, kanisa pia hata watu wengi wanalia nadhani
kwa sababu wanapata mguso ambao pengine kuna mambo walishapitia, pengine
wamekata tamaa yaani ile basi kama vile wanaona Mungu amewasahau lakini
niwaambie kuwa Mungu anatuambia tusishughulike sisi wenyewe tusije
tukafichaficha au tukajifanya hatutaki kuyataja, tumwambie waziwazi ndivyo
ninavyoomba yaani nikulisema linalonitatiza,” anasema.
Sarah K aliyeanza huduma ya uimbaji mwaka 1991 ambapo alitumia
lugha yake ya asili na kufanikiwa kutoa albamu tatu kwa lugha yake.
“Nina albamu kama tatu hivi za kilugha halafu mwaka wa 2000 ndio
nilitoa albamu ya kwanza iliyokuwa inaitwa Wamtumainio Bwana na Mwimbieni Bwana
nyimbo kama hizo. Halafu mwaka 2003 ndio nikatoa albamu ya Milele Daima na
ndani yake ndio kuna wimbo ‘Nasema Asante’.
“Hivyo ukijumlisha zote za Kiswahili na Kiingereza ni
Wamtumainio, Milele Daima, Adonai, Testimony na nyingine; na sasa nina Liseme
na nimetoa albumu nyingine mpya ya sita ambayo ni mpya.
“Hiyo ina siku kadhaa sasa kwa hivyo za Kiswahili ni sita na za
kilugha kama tatu hivi,” anasema.
Muimbaji huyo anasali katika kanisa la Anglikana ambapo mume
wake ni mchungaji na anasema: “Ombi langu ni kwamba namwamini Mungu nitaendelea
katika huduma yangu ya uimbaji hata kama nitakuwa na miaka 80 hata kama
nitakuwa na miaka 90.
“Nitaendelea kumwimbia Mungu na kuwa mnyenyekevu na mtiifu mbele
zake sio mbele za watu tu.
“Katika utunzi wangu ninamhusisha Mungu zaidi ya mimi mwenyewe
ninavyojiona “Siwezi kusema ooh kwa sababu nina albumu tisa au 10; yaani nina
ujuzi kabisa wa utunzi kwa hivyo simhitaji Roho Mtakatifu na simhitaji
Mungu-siwezi kumsahau Mungu.
“Ninawajenga watu mioyo yao; nitakuwa nawainua watu mioyo yao
ambao ni wadhaifu kwenye maeneo ambayo Roho Mtakatifu ananipa watasikia
wameinuka na kuwa na matarajio kwamba Mungu yupo na ataendelea kuwatendea
makuu-ni mengi tu wacha niachie hapo kwanza.”
Muimbaji huyo anawataka wasanii wachanga wasife moyo na
wafuatilie ndoto zao na maono yao kwa sababu kuna mambo mengi ambayo yanaweza
kupotosha uimbaji wao.
“Mambo mengi huja kwa mtindo kwamba umefika kumbe bado hujafika;
nitakutolea mifano miwili: hili linaweza kuzungumziwa kwa urefu sana katika
uimbaji, inaweza ikaja ukiwa mchanga halafu Mungu akakupa kibali sana mbele ya
watu kwa wimbo wako kupendwa na ukauzwa sana.
“Sasa hapo kikwazo kimoja kinaweza kukufanya ukarudi nyuma; ni
zile hela utakazozipata kutoka kwenye uimbaji ule zinaweza kukutikisa ukarudi
nyuma ukakosa kufuatilia yale maono yako uliyokuwa nayo au ahadi ulizoweka
mbele za Mungu.
“Unajua kuna ahadi zile uliweka wakati uko chini kabisa
ukamwambia Mungu, ‘Utakaponivusha, utakaponibariki nitafanya mambo kadhaa’; kwa
hivyo unajikuta umesahau.
La pili ni ile umaarufu wakati wimbo wako ume-‘hit’ ukajulikana
sana kuna ule umaarufu unaoupata kila mtu anakuita Sarah K, Sarah K kila mtu
anaongea juu yako redio zote zinakutaja; kwa hiyo hiyo umaarufu ukishaingia
ndani yako na ukaukubali kwamba wewe ni maarufu ndipo kiburi kitaanza kujiinua.
“Ni vema kuendelea kuwa mnyenyekevu tu daima na umshukuru Mungu.
No comments:
Post a Comment