KUMPENDA
JIRANI YAKO
Somo:
Luka
10
Katika somo hili tutaangalia zaidi
maagizo ya Yesu kuwa, kama kweli tunataka tuwe wafuasi wake, ni lazima tuoneshe
katika maisha yetu kiwango kisicho cha kawaida cha upendo kwa watu wengine.
Mahali pa kuanzia pa somo hili ni mfano wa Msamaria-mwema uliotajwa katika somo
letu lililopita. Tunapoangalia kwa ukaribu maneno ya Yesu katika Luka 10:30-37,
tunaona mambo kadhaa ya muhimu.
Kwanza, Yesu alichagua kumweka
Msamaria katika mfano huo, kwa kuwa Wasamaria walikuwa wakichukiwa na Wayahudi;
walikuwa wakionekana kama watu wa kudharaulika.
Pili, mtu aliyeshambuliwa na
wanyanganyi, hakusaidiwa ni watu wawili waliokuwa wakistahili kwanza kumhurumia
na kumsaidia. Makuhani waliokuwa wakitokana na kabila la Lawi, walikuwa
wakiwajibika katika Sheria ya Musa kuangalia afya na huduma kwa ujumla za Wana
wa Israeli, lakini hakuna kilichofanyika.
Ni Msamaria aliyeonesha upendo na
huruma, kwa kufanya mambo aliyofanya kusaidia. Alimwosha majeraha, akambeba mtu
huyu aliyeumizwa kwenye punda wake na kumweka mahali pa usalama kupumzika.
Mwishoni, ndiye aliyeweka mpango wa msaada zaidi kwa ajili ya kuendelea
kuhudumiwa.
Tunaposoma katika Injili juu ya
matendo mengi ya uponyaji yaliyofanywa na Yesu, waandishi mara nyingi
wanaongezea maneno, Yesu: ‘Alimwonea huruma’. Mfano upo katika Luka 7:11-15.
Yesu alipokuwa amewateua wanafunzi
wake wa karibu kumi-na-wawili, alianza kuwafundisha juu ya upendo, msamaha na
huruma. Kama ukifungua sasa nyuma kwenye Luka
6:17 utaona hayo kwa pamoja. Umati uliomsikiliza Yesu siku hiyo ulikuwa mkubwa
sana, na wengi walikuwa wamekuja kutoka mbali sana kumwona. Walio wengi
walikuja ama kuponywa, ama kuona matendo ya Yesu ya kuponya. Walikaa hapo muda
wote kusikia mafundisho yake kuhusu ufuasi wa Kikristo, na tutafanya na sisi
hilo, tukitazama zaidi mstari ya 27 mpaka na 36.
Hakuna hasa linaloshangaza; tunalosoma
katika Injili ya Luka ni kama lile lile tulilolisoma katika Injili ya Mathayo,
katika somo letu lililopita. Ujumbe huu ni wa maana mno kiasi kwamba unarudiwa
mara nyingi katika Biblia. Kile kinachoanza kama wazo katika akili zetu, mara
nyingi kinageuka kuwa tendo, kwa hiyo sheria ya Yesu inahitajika kwanza iongoze
katika kufikiri kwetu, ndipo hatimaye inapoweza kutawala matendo yetu.
Tunapoonesha upendo wa huruma kwa mtu mwingine, tunafanya hivyo kwa matendo
yetu.
Muda mfupi kabla Yesu hajaondoka
katika kile Chumba cha Juu, alipofurahia mlo wa pamoja na wanafunzi wake kabla
ya kufa, uliirudia tena hii amri ya muhimu kipekee kuhusu upendo. Tunaiona
katika Injili ya Yohana 13:34, 35.
Maneno yake yanahitaji kuzingatiwa kwa
umakini kwa kuwa, upendo wa Kikristo unaooneshwa na wanafunzi wake, unatakiwa
uwe mkubwa kama ule uliooneshwa na Kristo mwenyewe kwa hao wanaume na wanawake
wa enzi yake, na wale wote ambao wangefuata katika nyakati zote.
Alionesha upendo wake kwa kujitoa kwa
hiari kufa msalabani, ili wote wanaomfuata, wanaoonesha imani ya kweli, waweze
kupata fursa ya kuwa na uzima usio na mwisho katika Ufalme wake katika dunia
hii. Hebu angalia Yohana 15:9-14 na uone vile amri hii inavyorudiwa katika
mstari wa 12 na wa 17.
Petro alipojitetea kuwa kamwe
hatamwacha Yesu (Yohana 13:36-38), Yesu alimwambia, kabla jongoo hajawika
(yaani kabla hakujakucha), angemkana Bwana wake Yesu mara tatu. Lilipotokea
hivyo kama Yesu alivyotabiri, Petro alitahayari, lakini alijifunza somo kuwa,
kumpenda Bwana Yesu hakuwi kitu kirahisi mtu anapobanwa.
Baada ya Yesu kufufuka, aliwakuta
wanafunzi wake upande wa kaskazini katika Galilaya, mahali ambapo saba kati yao
walikuwa wameamua kuchukua mashua na kwenda kuvua. Walijiunga na Yesu ufukweni
mahali ambapo alikuwa ameandaa chakula cha mkate na samaki (Yoh. 21:9). Ni
jambo la muhimu kuwa, Yesu alikuwa amewaonesha huruma yake umati ule wa watu
elfu tano na baadaye elfu nne kwa kuwalisha kwa muujiza mikate na samaki.
Baada ya kula hapo ufuweni mwa Bahari
ya Galilaya, Yesu alilihitimisha somo lake la upendo kwa kumuuliza Petro mara
tatu juu ya upendo wake kwa Bwana wake. Yesu aliendelea kwa kuongeza maneno
mengine kwenye maelekezo yake ya awali (ms. 15-18). Ilikuwa kwamba, kila mara
Petro aliposema kuwa alimpenda Yesu, alipewa amri na majukumu ya: kulisha
wana-kondoo, kuchunga kondoo, kulisha kondoo wa Yesu.
Katika miaka ya awali ya kanisa jipya
(Ukristo), kulikuwa na wana-kondoo wengi (wafuasi wapya) wa kutunzwa. Eklesia
nyingi zilipoanzishwa katika maeneo mengi ya Israeli na nchi zingine, majukumu
yalibadilika kukawa na haja ya ulezi kwa jumuia zilizokuwa zimeanza (kondoo).
Paulo aliitumia lugha hii hii katika ujumbe wake alipokuwa akiwaaga wazee
katika eklesia ya Efeso (Matendo 20:28, 29).
Mtume Yohana naye alijifunza somo hili
la muhimu sana
la upendo kutoka kwa Yesu. Alipokuwa akining’inia msalabani, Yesu alisema na
Yohana na kumpa jukumu juu ya mama yake, Mariamu (Yohana 19:26, 27).
Miaka kama 50 baadaye Yohana aliandika
Waraka aliokusudia usomwe katika Eklesia zote. Katika huo alieleza kwa kifupi
sheria ya upendo wa Kikristo (1 Yohana 4:7-21). Soma mistari hii kwa makini
maana ni ya muhimu sana, na hasa katika nchi ambazo kuna chuki za kutisha kati ya
kundi moja la kijamii na kundi lingine, wazimu wa kuangamizana kati ya kabila
moja na jingine, vita kati ya eneo moja na jingine, mji na mji, kijiji na
kijiji, chuki kati ya familia na familia, ndugu na ndugu.
Maneno ya Yohana ni thabiti na
hayaachi shaka lolote katika mawazo yetu. Haiwezekani kwa mfuasi wa Kristo
kusema kuwa anampenda Mungu, na wakati huo huo akawa na chuki kwa Wakristo
wenzake moyoni mwake. Kama mtu anasema
anampenda Mungu na anamchukia ndugu yake, ni mwongo. Hakuna namna ya kuweza
kuyakwepa maneno haya, na kwa wale wanaotaka kubatizwa au wale waliobatizwa
hivi karibuni, hili ni fundisho la muhimu sana.
Kuna mambo mengi sana ya sisi
kukumbuka kutoka kwenye maneno hayo kiasi kwamba, ningependa nitumie sehemu
iliyobaki ya somo hili kuyaangalia kwa undani:
1.
Mstari
wa 7: “Pendo latoka kwa Mungu” – hili lina maana kuwa katika uumbaji, uwezo wa
kuonesha upendo wa kujitoa ulijengwa ndani yetu kwa namna Mungu alivyotuumba.
Anatutaka tuuitikie upendo wake na upendo wa Yesu kwetu.
2.
Mstari
wa 10: Mungu alimtuma Yesu awe dhabihu kwa ajili ya dhambi zetu. Hiki ni kipimo
cha upendo wake kwetu.
3.
Mstari
wa 11: Kwa kuwa Mungu anatupenda, ni lazima tuoneshe upendo kwa wengine.
4.
Mstari
wa 12: Tunapouonesha huu upendo unaotoka kwa Mungu kwa watu wengine, kuna kitu
kinachomhusu Mungu ndani ya kila mmoja wetu.
5.
Mstari
wa 17: Kama ni kweli kwamba tunajisikia kuwa tumeweza kuonesha upendo huo wa
Mungu kwa wengine, basi hatuhitaji kuwa na hofu ya hukumu siku ya kurudi kwa
Yesu.
6.
Mstari
wa 10: “Pendo lililo kamili huitupa nje hofu”. Kuna faida ya uhakika kwa wale
wanaoweza kuuonesha upendo wa namna hii.
7.
Mstari
wa 20 na 21. Hii ni mistari ambayo tumekwisha itazama lakini kwa sababu ya
kukua kwa chuki na mauaji kati ya watu katika nchi nyingi za dunia, nataka hasa
nisisitize umuhimu wa ujumbe huu.
Hatuwezi kumpenda Mungu na kumchukia
kaka au dada yetu. Kwanza Yohana hapa anaongea na wafuasi wa Yesu; watu
waliobatizwa. Hakuna kabisa sababu ya kuwa na uadui kati yetu tunapokuwa
tumebatizwa.
No comments:
Post a Comment