JUKWAA LA WAKRISTO TANZANIA
TAMKO LA JUKWAA LA WAKRISTO TANZANIA KUHUSU MCHAKATO WA
KATIBA
Sisi, wajumbe wa Jukwaa la Wakristo Tanzania,
tuliokutana tarehe 27 hadi 28 Agosti, 2014, Dar es salaam , tumepata fursa ya
kutafakari, kujadili na kujielimisha kwa kina yaliyomo katika Rasimu ya pili ya
Katiba na mjadala unaoendelea katika Bunge Maalum la Katiba.
Baada ya mjadala wa kina, tunatoa tamko letu kama ifuatavyo:
- Tunaipongeza
Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilikusanya Maoni ya
WANANCHI kuhusu mabadiliko hayo na kutuletea Rasimu yenye maoni mengi ya
Watanzania bila kujali dini zao, upande wa Muungano walikotoka, hali zao
za kimaisha, jinsi na kabila.
- Pia
tunaipongeza Tume kwa kuandaa nyaraka na kumbukumbu mbalimbali kama
Randama, Nyaraka zenye maoni ya wananchi, picha, tafiti mbalimbali na hata
orodha ya watu walioshiriki kutoa maoni katika Tume. Tume pia iliweza
kuandaa Tovuti iliyokuwa na kumbukumbu za Tume na Maoni yote yaliyotolewa.
Kazi hii ni ushahidi kuwa Tume iliandaa Rasimu kwa weledi na kwa mujibu wa
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwa kuzingatia maoni ya WANANCHI.
- Tume
imedhihirisha kuwa, ilitenda KIZALENDO na, kwa mantiki hiyo, wajumbe wote
bila kujali vyama vyao, dini zao na upande wa Muungano walikotoka,
waliweza kujadili kwa uwazi na kweli na mwisho wakaridhiana katika kila
Ibara iliyopendekezwa. Hili linatufundisha kuwa Katiba ni MARIDHIANO na si jambo la
maslahi ya kisiasa, bali ni suala la maslahi ya WANANCHI.
- Tunaamini
kuwa kila Mjumbe wa Kamati ya kukusanya maoni ya WANANCHI aliheshimu kiapo
chake na hivyo kufanya kazi waliyokabidhiwa kwa uaminifu na uadilifu na ya
kwamba hawakushawishiwa au kupokea rushwa kutoka kwa kundi, dini au chama
chochote cha siasa wakati wa zoezi hili.
Baada ya Tume kuwasilisha Rasimu kwenye Bunge Maalum la
Katiba, Taifa likaanza kushuhudia “uasi wote na uovu wa wanadamu wapingao
kweli kwa uovu” (Warumi 1:18). Katika mijadala ya Bunge Maalum la
Katiba (BMK) yakaanza kujitokeza mambo mengi yasiyo ya maslahi kwa WANANCHI, na
ukiukwaji wa sheria na kanuni. Mambo kadhaa yanadhihirisha hili:
- Tovuti
ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilifungwa bila sababu za msingi kutolewa
wakati mchakato unaendelea. Hali hii imefanya zile nyaraka na kumbukumbu
zilizoandaliwa kwa ajili ya rejea na kuwezesha mjadala wa Rasimu ya Katiba
kuendelea katika mwanga na ufahamu wa nyaraka hizo kutowezekana kabisa.
Kwa sababu hiyo, tumeona Bunge Maalumu la Katiba likiendelea kupotosha
takwimu na taarifa mbalimbali ambazo WANANCHI hawawezi kuzipata kwa ajili
ya kuoanisha baina ya kinachojadiliwa Bungeni na kilichomo katika Rasimu na
viambatanisho vyake vyote. Tunajiuliza jambo hili limefanywa na nani na
kwa maslahi ya nani?
- Bunge
la Katiba limeshindwa kusimamia Kanuni kama ambavyo zilipendekezwa na
kuridhiwa na wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba. Kushindwa huku kusimamia
kanuni kumesababisha vurugu ndani ya Bunge Maalumu na kumekwamisha
matarajio ya wananchi kupata Katiba bora ya nchi yetu.
Matumizi ya ubabe na wingi wa Wabunge wa Chama Tawala (CCM), badala ya
Kanuni za Bunge na maridhiano, kumefanya mchakato wa Katiba kuhodhiwa na
Chama Tawala dhidi ya maslahi ya WANANCHI.
- Mijadala
katika Bunge Maalumu la Katiba imekuwa ya kejeli, matusi, vitisho, ubabe
na kupuuza hata kupotosha maoni yaliyotolewa na Wananchi kwa Tume. Hali
hii imelifanya Bunge Maalumu la Katiba kupuuzwa na hivyo kupoteza heshima
na hadhi yake. Matokeo yake baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba wakaamua
kususia vikao vya bunge na wengine kuendelea, bila kukumbuka kuwa KATIBA
NI MATOKEO YA TENDO LA MARIDHIANO NA SI SUALA LA MASLAHI YA KIKUNDI CHA
WATU WACHACHE.
- Hatua
iliyofikiwa ni dhahiri, Mjadala wa BMK unaoendelea umeondoa kwa kiasi
kikubwa maoni yaliyotolewa na wananchi kuhusu muundo wa Muungano,
kupunguza mamlaka ya Rais, uwajibikaji na uwajibishwaji wa wabunge, ukomo
wa ubunge, n.k., na kuwezesha maoni na maslahi ya Chama Tawala kwa uongozi
wa kikundi cha wanasiasa wachache wasio na uaminifu na uadilifu wa kutosha
kuwekwa kama mapendekezo ya Katiba mpya kwa nia ya
kulinda maslahi binafsi au ya makundi na kuhalalisha ukiukwaji mkubwa wa
sheria, kanuni na maadili ya uongozi bora.
Baada ya kujadili na kuona haya na mengine mengi, Jukwaa la
Wakristo Tanzania lina maoni yafuatayo;
1. Kwamba Serikali (Wizara ya Katiba na Sheria) irudishe
tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na nyaraka zake zote kwa ajili ya wananchi
kuendelea kuona kazi waliyoifanya, kujifunza na kujadili Rasimu ya Katiba kwa
uwazi.
2. Kwamba maoni ya wananchi hayawezi kufutwa na kudharauliwa
na Chama Tawala. Hivyo basi, Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea lijadili na
kuboresha tu maoni yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na sio kufanya mabadiliko
katika Katiba ya mwaka 1977.
3. Kwamba mchakato wa Katiba usimamishwe ili kupisha
majadiliano, maelewano na maridhiano muafaka, uchaguzi mkuu na wa serikali za
mitaa. Na mabadiliko ya Katiba ya 15 ya mwaka 1977 yafanyike kuwezesha chaguzi
kufanyika kwa uwazi na haki. Pia, kuweka kifungu kitakacholinda Rasimu ya pili
na kumtaka kiongozi ajaye kuendelea na mchakato wa Katiba.
4. Kwamba baada ya Bunge Maalum la Katiba kuanza shughuli
zake tena, Mwenyekiti wa Bunge hilo afanye kazi kwa mujibu wa kanuni na Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba badala ya kutumia ubabe na kiburi cha wingi wa wajumbe
wa Chama cha Mapinduzi katika Bunge la Katiba.
5. Kwamba wananchi waendelee kusoma na kujadili maoni
yaliyoko katika Rasimu ya pili ya Katiba, na kufuatilia kitakachokuwa
kinajadiliwa kwenye Bunge la Katiba ili kuwawezesha kupiga kura ya maoni wakiwa
na uelewa wa kutosha kabisa kuhusu ni nini kipo kwenye “Katiba
inayopendekezwa”. Wananchi pia wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwa nia ya
kuwawezesha kupiga kura ya maoni.
6. Kwamba tunaomba Tume ya Mabadiliko ya Katiba ihuishwe na
kupewa mamlaka kisheria ili kuiwezesha kujibu maswali yanayojitokeza na kutoa
ufafanuzi kwa Bunge Maalumu la Katiba na wananchi kwa jumla hadi Katiba Mpya
itakapokamilika na kukabidhiwa rasmi.
Jukwaa la Wakristo Tanzania na Watanzania wote wanaoitakia
nchi yao mema, tunakuomba Mheshimiwa Rais kwamba AMANI ya nchi yetu sasa imo
mikononi mwako hasa katika kipindi hiki cha kuandikwa kwa Katiba Mpya.
Tunakuomba uahirishe mchakato unaoendelea ili uepushe ishara za aina mbalimbali
za kuanzisha sintofahamu nchini mwetu na hali yoyote inayoweza kuathiri vibaya
mshikamano, umoja na amani ya Taifa letu.
Ifahamike kuwa WANANCHI wa Tanzania wako juu ya Wajumbe wa
Chama cha Mapinduzi. Kwa mantiki hiyo, tunakuomba uepushe WANANCHI wa Tanzania
kuhamasishwa kukikataa Chama cha Mapinduzi kwa kuwa tu Chama hicho kimeyapuuza
na kimekataa Maoni yao waliyotoa kwa dhati baada ya kuaswa na kuhimizwa kufanya
hivyo na viongozi wa nchi.
“Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao,
Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wafanye yasiyowapasa. Wamejawa na
udhalimu wa kila namna, uovu na uuaji, na fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya,
wenye kusengenya, wenye kusingizia, wenye kumchukia Mungu, wenye jeuri, wenye
kutabakari, wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao, wasio
na ufahamu, wenyekuvunja maagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema; si
hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao”. (Rejea Warumi 1: 28-32)
IKUMBUKWE KUWA RASIMU YA PILI YA KATIBA NI WARAKA HALALI
NA RASMI NA NDIYO MAWAZO YA WATANZANIA NA TUNAHIMIZA KUWA KATIBA NI YA WANANCHI
NA INAHITAJI MARIDHIANO NA SIO UBABE.