HII NDIO HISTORIA YA MWANAMUZIKI WA NYIMBO ZA INJILI REBECCA MALOPE
REBECCA Malope wengi akijulikana kama Malkia wa
muziki wa injili Afrika amezaliwa 1968 katika kijiji cha Lekazi karibu na mji
wa Nelsprut, Mpumalanga.
Historia ya mwimbaji huyo ambayo si nzuri kimaisha kwani
Malope hakuendelea sana katika elimu na ni mambo machache sana yanafahamika
kuhusiana na enzi za utoto wako.
Akiwa katika umri mdogo Malope alipata ugonjwa uliopelekea
kutoweza kutembea na madaktari walidhani asingeweza kutembea tena katika maisha
yake .
Familia yake ilikuwa masikini sana na ndipo yeye na dada
yake Cynthia waliamua kukimbilia katika jiji la Johannesburg kitongoji cha Evaton
kwa ajili ya kutafuta kazi kujikimu na maisha.
Mwaka 1986 Malope akiwa na miaka 21 alishirika kwenye
mashindano ya kutafuta vipaji vya uimbaji yaliyojulikana kama ‘Shell Road to
Fame’ lakini hakufanikiwa kufika mbali.
Malope hakukata tamaa ndipo mwaka uliofuata alishiriki tena
na kuibuka mshindi na wimbo wa ‘Shine on’ ushindi huo ulimsogeza mbali sana
kimuziki na ndipo alipokutanishwa na muandaaji mashuhuri Sizwe Zako na akapata
meneja wake wa kwanza akijulikana kwa jina la Peter Tladi.
Albamu yake ya kwanza ilikuwa na nyimbo za kidunia, albamu
hiyo ambayo haikufanya vizuri sokoni na ndipo alipoamua kujiingiza moja kwa
moja kwenye muziki wa injili.
Alipata ushirikiano mkubwa sana kutoka radio mbalimbali kwa
nyimbo zake za injili kitu ambacho hakikuwa kawaida sana Afrika Kusini.
Mwaka 1990 Rebecca alishinda tuzo ya mwanamuziki bora wa
kike wa Afrika Kusini,na mwaka 1993 ilikadiriwa watu zaidi ya milioni moja
walimpigia kura kama mwanamuziki bora wa kike kwenye Coca Cola Full Blast Music
Award Music Show na alishinda kwa mwaka huo na 1994 pia. Kwenye mauzo, Album
zake zote kumi za kwanza ziliingia kwenye hadhi ya dhahabu.
Katika kipindi chote nakala zaidi ya milioni 2 zilikuwa
zimeshauzwa sokoni.Mwaka 1995 kwenye CD yake ya Shwele Baba nakala zadi ya
milioni moja ziliuzwa ndani ya wiki tatu toka uzinduzi wake na hii iliweka
rekodi ya aina yake katika historia ya soko la muziki Africa kusini.
Mwaka 1996 haukuwa mwaka mzuri kwa Rebecca kwani alimpoteza
baba yake mzazi, kaka yake na dada yake. Wote walifariki katika mazingira ya
kutatanisha wakifuatana.
Lakini hili halikumfanya Rebecca kukata tamaa na kuacha
huduma bali alisonga mbele na kazi hiyo akijipa moyo na kuamini ni mpango
kutoka kwa Mungu mwenyewe na hataacha kumtumikia.
Rebecca anasema siri ya mafanikio yake ni kujituma, kuwa na
malengo na kufanya kazi kwa bidii akimshirikisha Mungu hayo ndiyo yaliyomfanya
kutawazwa Malkia wa muziki wa injili Afrika huku wengi wakimfananisha na
marehemu Brenda Fassie.
Kati ya mwaka 1995 na 2004 Rebecca amezunguka ulimwenguni
akiwa na bendi ya Pure Magic akimtukuza Mungu kwa njia ya uimbaji.
Mwaka 2003 Malope alitunukiwa udaktari wa heshima kutoka
chuo kikuu cha Natal kwa mchango wake mkubwa kwa jamii na muziki nchini Afrika
kusini, na Desemba mwaka huo huo alishinda tuzo ya Kora kwa upande wa
mwanamuziki bora wa Injili.
Katika wanamuziki ambao alishirikiana nao kwa karibu sana na
wamekuwa na mchango mkubwa kwake ni pamoja na marehemu Vuyo Mokoena.
Mwaka 2004 Malope alianzisha kipindi chake katika runinga
kikiitwa ‘Gospel time’ ambacho kinafanya vizuri sana.
Mwaka huu februari 25 Malope amerekodi nyimbo za live katika
jiji la Pretoria hiyo ikiwa ni albamu ya 32.
Baadhi ya Tuzo ambazo Dkt. Rebecca Malope amewahi kutunikiwa
ni 1994 mwimbaji bora, 1997 albamu bora sokoni iliyoitwa Uzube Nam, 1998
muimbaji bora wa nyimbo za injili Afrika na albamu bora katika mauzo iliyoitwa
Angingedwa.
Nyingine ni 1999 muimbaji bora wa kike na muimbaji bora wa
injili Afrika kupitia albamu ya Somlandela, 2002 msanii bora wa nyimbo za
injili akishinda na wimbo wa Sabel Uyabizwa, 2003 msanii bora Afrika kupitia
wimbo wake wa Iyahamba Lenqola na 2004 msanii bora wa mwaka kwa wimbo wake
Hlala Nami.
Huyo ndiyo Rebecca Malope ambaye ni kipenzi cha Rais wa
kwanza wa frika Kusini Nelson Mandela na rais wa sasa Jacob Zuma ambaye
amepitia tabu na changamoto nyingi katika maisha.
No comments:
Post a Comment